Friday, July 11, 2014

Fredrick sumaye asema yeye ndo tumaini pekee kwa watanzania


WAZIRI Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye,
amesema yeye ni tumaini la Watanzania na
mpambanaji wa vita dhidi ya maovu.

Kutokana na hali hiyo, amesema ni jemadari
hodari aliyeungana na askari wapiganaji
hodari wa vita ambao wataleta ushindi usio na
shaka.

Kauli hiyo aliitoa jijini Mwanza jana, katika
hotuba yake ya uzinduzi wa taasisi ya Vijana
ya Tanzania Youth (TYDC), ambako alipinga
hatua ya baadhi ya wanasiasa kununua wapiga
kura kwenye uchaguzi na kufanikisha kitendo
hicho ni sawa na uroho wa madaraka.

Alisema hali hiyo ni hatari, kwani wanasiasa
wa aina hiyo wanapaswa kuangaliwa kwa
umakini wa hali ya juu, wanaweza
kulisambaratisha Taifa.

Sumaye ni mmoja wa makada sita wa CCM
waliopewa onyo kutokana na kile kilichoelezwa
kuanza kampeni za kuwania urais kabla ya
wakati.

Akizungumza na MTANZANIA baada ya
uzinduzi wa taasisi hiyo, Sumaye alisema yupo
tayari kugombea urais iwapo ataombwa
kufanya hivyo.

Akijibu maswali kwa waandishi wa habari,
alisema dhamira yake katika kujitosa kuwania
urais ipo, lakini pale atakapoombwa
kugombea.

“Nikiombwa kugombea urais nitagombea, hilo
wala halina tatizo…na mjue kutangaza nia siyo
kosa kwa mujibu wa kanuni za CCM, ila kosa
ni kufanya kampeni kabla ya muda, wakati rais
anapomaliza muda wake wagombea wengi
hujitokeza kuwania nafasi hiyo, sasa hata
mimi nikiombwa nitagombea,” alisema
Sumaye.

Sumaye, anayetajwa kuwa miongoni mwa
wanasiasa ndani ya CCM wanaotaka kuwania
urais mwaka 2015, akizungumza katika
uzinduzi huo wa TYDC, alisema kuna watu
wamekuwa wakitumia nguvu ya fedha kusaka
madaraka na kuwafananisha na watu wafupi
wanalazimisha kupanda juu ya stuli ili
waonekane mbele ya jamii kwa kutumia nguvu
kubwa ya fedha.

Alisema watu hao ni hatari iwapo
wakichaguliwa na kushuka juu ya stuli kwa vile
hawataonekana tena kuwasaidia wananchi na
kubainisha wamekuwa wakiwatumia vijana
vibaya ili kukidhi malengo yao binafsi,
yakiwemo ya kisiasa.

Katika kongamano hilo, Sumaye alitangaza
kuwa mlezi wa vijana nchini na kuwaahidi
maisha ya matumaini kwa miaka ijayo.

“Mimi nataka niwe mlezi wa vijana wa
Tanzania nzima ili wawe na maisha ya
matumaini. Ninyi vijana mtu akiwaleteeni hela
chukueni kuleni halafu mnamchagua
mwingine.

Yaani hata Sumaye akileta msikatae
hela, chukueni kuleni msimchague, maana mtu
anayetumia nguvu ya fedha kusaka madaraka
ya Serikali za Mitaa, udiwani, ubunge na hata
urais huyo hafai na ni dhaifu,” alisema
Sumaye, huku akieleza hakuja kwenye
kongamano hilo kwa sababu za kisiasa.

Aliwaasa vijana wote, hususan waliopo
masomoni wasidanganyike wala kutegemea
kupata ajira za ofisini na kwamba wasiopata
ajira wasikubali kutumiwa kisiasa, vijana
watakaotumiwa watakuwa wamejiunga katika
kundi la wala rushwa na wapokea rushwa,
watakuwa wamejiunga kwenye kundi la
mafisadi na la maangamizi kwa taifa.

Alisema kwamba vijana ni jeshi muhimu la
taifa kwa maslahi ya taifa na wananchi wake
na siyo jeshi la kuleta maafa katika jamii,
hivyo atakuwa mlezi wa vijana kwa mambo
yote na sifa anayoipenda ni mtu kuwa
mzalendo wa kweli, kusimamia haki ya umma
na siyo maslahi binafsi.

Alisema kwamba, hivi sasa Watanzania
wanaelekea kwenye uchaguzi na fedha nyingi
zinatembezwa kwa vijana ili watoa rushwa
wachaguliwe katika nafasi wanazoomba na
kudai siku hizi kumeibuka mtindo wa watoa
fedha kuitwa wakarimu na wasiotoa kuhonga
wao huitwa wachoyo.

“Mliponitaka niwe mlezi wenu nilikubali kwa
sababu mimi ni mpambanaji wa vita dhidi ya
matatizo na maovu hayo ambayo TYDC
imeyaweka kama malengo yake makuu.

“Hivyo niliona nimepata wapiganaji wenzangu
katika vita hii na kwa bahati nzuri wapiganaji
wenyewe ni vijana ambao ni wengi, ni wenye
nguvu na ndio wenye uchungu na nchi yao.

"Mimi ninawaahidi kuwa mmempata jemadari
hodari wa kuongoza vita hii na yeye jemadari
amepata askari mashujaa wa kupigana vita
hiyo,” alisema.

Alisema muunganiko huo wa wawili wa
jemadari hodari na askari wapiganaji hodari
wa vita utaleta ushindi usio na shaka.

“Kama unavyoambiwa wewe na wenzako
wengine wasiokuwa na mahesabu nao
huambiwa vivyo hivyo. Lakini la msingi ujue
kuwa kama mtu anatumia njia hizo za mkato
kutaka kuingia madarakani, huyo mtu
hajiamini na wala hana uhakika na uwezo
wake wa kumudu hayo madaraka
anayoyatafuta, vinginevyo asingehangaika
kuhonga watu,” alisema Sumaye.

Awali akimkaribisha Sumaye kuzungumza na
halaiki ya vijana zaidi ya 300, Mwenyekiti wa
TYDC, Lengai Thomas Ole Sabaya, alionekana
wazi kumpigia ‘debe’ Sumaye katika harakati
zake za kisiasa, kwa kusema wakati wa utawala
wake na Mkapa fedha ya Tanzania ilikuwa na
thamani kuliko ilivyo leo hii.

Sumaye alikuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10
katika Serikali ya Rais Benjamin Mkapa.

Februari 18, mwaka huu, Chama Cha
Mapinduzi (CCM), kupitia Kamati Ndogo ya
Udhibiti na Nidhamu katika kikao chake
ilipendekeza kuchukuliwa hatua za kinidhamu
kwa makada wake ambao wameanza kampeni
ya kuwania urais wa mwaka 2015.

Uamuzi huo wa kamati hiyo ya maadili
ulibarikiwa na Kamati Kuu (CC) ya CCM,
iliyokutana Februari 17, mwaka huu mjini
Dodoma, chini ya Mwenyekiti wake, Rais
Jakaya Kikwete.

Makada waliopewa adhabu ya mwaka mmoja
kwa tuhuma za kuanza kampeni za kuwania
urais kabla ya wakati ni January Makamba,
Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa,
Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye,
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe.

Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Uhusiano na Uratibu) Steven Wassira pamoja
na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini
ambaye ni Mbunge wa Sengerema, William
Ngeleja.

Katika adhabu hiyo, makada hao walizuiwa
kujihusisha na masuala ya kisiasa ndani ya
chama hicho kwa miezi 12, huku mwenendo
wao wa kisiasa ukifuatiliwa chini ya uangalizi
mkali katika kipindi chote cha kutumikia
adhabu hiyo.

Kabla ya adhabu hiyo, makada hao waliitwa na
kuhojiwa na Kamati Ndogo ya Maadili ambayo
iliwatia hatiani kwa kutumia Kitabu cha Kanuni
ya Uongozi na Maadili ya CCM, toleo la
Februari 2010, Ibara 6 (7)(i).

No comments:

Post a Comment

Total Pageviews