Friday, July 4, 2014

Wizara ya Afya ya waonya madaktari feki

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii nchini
Tanzania imewaonya watu wanaojiita
madaktari na maprofesa bila ya kuwa na sifa
hizo huku wakidai kuwa na uwezo wa kutibu
magonjwa yasiyotibika ukiwemo ugonjwa wa
Ukimwi na kisukari.

Mganga mkuu wa serikali Dkt Donnan
Mmbando ametoa onyo hilo jijini Dar es
Salaam jana, na kufafanua kuwa wenye haki ya
kujiita hivyo kwa mujibu wa sheria na kanuni
zinazosimamia tiba asili na tiba mbadala
nchini Tanzania, ni wale tu wenye sifa
zinazotambulika na mamlaka mbalimbali za
serikali.

Dkt Mmbando amesema inashangaza kuona
watu wakijitangaza na kujinadi eti ni
madaktari na wana uwezo wa kutibu
magonjwa hayo na mengine ambayo
yameshindikana ilhali sio kweli bali ni njia za
kijanja za kutaka kujipatia pesa.

Aidha, Dkt Mmbando amesema katika
kuhakikisha dawa za tiba asili na tiba mbadala
zinatolewa kwa mujibu wa viwango
vinavyotambulika kisheria, wizara inakamilisha
taratibu kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda
kitakachokuwa na jukumu la kusindika dawa
zote za asili ili ziwe katika mwonekano na
viwango vya kisasa.

Usindikaji huo kwa mujibu wa Dkt Mmbando,
utafanana na dawa zinazotumiwa katika
hospitali na vituo vya huduma za kisasa, hatua
itakayowafanya wananchi waachane na
kuchemsha mizizi na kunywa katika hali
ambayo hairidhishi kiafya.

No comments:

Post a Comment

Total Pageviews